MKOMAINDO WAPATA NIRA PAMPU
01.02.2006 - Shule ya msingi ya Mkomaindo iliyopo wilayani Masasi mkoani Mtwara wamepata msaada wa pampu ya kisima cha maji yenye urefu wa mita 12 kutoka kwa Rais wa Finland mheshimiwa Tarja Halonen.
Pampu hiyo yenye thamani ya millioni mbili na laki tano iliyotolewa mwaka 2003, ilikabidhiwa katika ofisi ya Mkurugenzi wa wilaya ya Masasi kwa niaba ya Mh. Tarja Halonen na shirika la Msaada wa Maendeleo ya Michezo tarehe 28 Januari 2005 na kusimikwa kwa msaada wa Halmashauri ya wilaya, Kamati ya maendeleo ya shule na jamii inayozunguka shule hiyo mnamo mwezi Oktoba.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa pampu hiyo, mwakilishi wa Wizara ya Mambo ya Nje kitengo kinachoshughulikia sera na mashirika yasiyo ya kiserikali nchini Finland, Bi Riikka Otsamo aliwapongeza wanafunzi, uongozi wa shule, wanakijiji pamoja na Halmashauri ya wilaya kwa juhudi zao kubwa kwa kusimika pampu hiyo. Aliwaasa waitunze kwani pampu hiyo si ya Rais wa Finland bali ni mali ya shule na ya Jamii inayozunguka shule hiyo.
Uhaba wa maji ni tatizo linalo sumbua shule nyingi wilayani Masasi. Shirika la msaada wa maendeleo ya michezo wa kishirikiana na idara ya maji wilaya ya Masasi walizunguka kwenye baadhi ya shule wilayani hapo ili kutanabahi shule zenye vina vya maji vyenye urefu usiozidi mita 12 na Mkomaindo ilionekana kuwa na kina kinachowezesha upatikanaji wa maji kwa kipindi cha mwaka mzima.
Sherehe hizo za uzinduzi zilipambwa na mechi ya mpira wa miguu wa wasichana kati ya timu ya FC Vito Malaika Masasi na timu ya wasichana ya shule ya Mkomaindo na matokeo yalikuwa 3 kwa FC Vito Malaika kwa 0.
|